ILULA YETU

ILULA YETU
HOME: ILULA YETU BLOG

Jumamosi, 10 Juni 2017

Meya wa Jiji la Arusha Amtaka Mkuu wa Mkoa Amuombe Radhi

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiOmEdbmM8osV5X4ENwwYaQm69EhDdVj1Qxz1Y4ySgiUtrXlu1OCMatjTj6t-wIcCu7M6wPcy8KxwsiB2gLFcWuwLvG9qThyphenhyphenWurT6CHdzHwK6EGgAKAHwfDBWvC6yJ8m5YKiZu5G0IEieOX/s1600/1.JPGMeya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ametoa siku saba kwa  Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amuombe radhi kwa kosa la kumuweka ndani wakati alipokuwa anakabidhi rambirambi kwa wazazi waliofiwa kwenye ajali ya gari la Shule ya Msingi Lucky Vincent.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake jana Ijumaa, Lazaro alisema mpaka sasa ameshindwa kuelewa ni kwanini mkuu huyo aliagiza meya pamoja na wenzake wakiwemo viongozi wa dini, madiwani, wawakilishi waliotoa rambirambi na mwenye shule kukamatwa na Jeshi la Polisi na kuwekwa ndani.

"Mimi sikuwa na shida na RC na kitendo cha kumuweka ndani kiongozi wa dini, paroko, kiongozi wa dini ya Kiislamu ni kitendo ambacho si cha kibinadamu na anapaswa aombe radhi umma,"alisema.

Pia, alimtaka kutafakari nafasi yake na kuona kuwa anafaa kuendelea kuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha kwasababu ameonyesha kuwatumikia wananchi ambao hawaheshimu.

"Hana heshima na mbunge, madiwani, watu wenye degree zao, haheshimu viongozi wa dini halafu bado anataka uongozi,"alisema.

Jumamosi, 6 Mei 2017

Yanga, Prisons kumekucha

View CommentsMABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Yanga leo wanashuka dimbani kuivaa Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi hiyo kusaka pointi tatu muhimu kuelekea kwenye harakati zao za kutetea taji hilo.
Mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga imetoka kupoteza mchezo wake wa nusu fainali Kombe la Shirikisho la Azam kwa kutolewa na Mbao FC baada ya kufungwa bao 1-0.
Huenda ikautumia mchezo huo kutafuta ushindi na kupoza machungu ya mashabiki wake baada ya kushindwa kusonga mbele hatua ya fainali ya michuano ya shirikisho. Katika mchezo wa raundi ya kwanza, Yanga ilishinda kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya bao 1-0.
Pia, katika mchezo wa robo fainali FA, Yanga iliwafunga tena Prisons mabao 3-0. Mchezo wa leo hautakuwa rahisi kwa pande zote Yanga ambaye anataka kupata pointi zitakazomsaidia kukimbizana na Simba kileleni kwenye msimamo, lakini pia, Tanzania Prisons ambao wana pointi 31 zisizotosha kuihakikishia kubaki salama.
Yanga yenye pointi 56 iwapo itashinda itafikisha 59 na kubakiza michezo minne mkononi, lakini kuna nafasi kubwa ya kupanda kileleni akiongoza kwa magoli mengi ya kufunga lakini iwapo Simba yenye pointi sawa na hizo 59 itashinda kesho dhidi ya African Lyon, basi Yanga itashuka nafasi ya pili.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema wachezaji wote wanaendelea vizuri na wapo tayari kwa mchezo huo. “Tunashukuru Mungu wachezaji wote waliokuwa Mwanza wanaendelea vizuri, tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi,”alisema.
Aidha, Azam FC inayoshika nafasi ya tatu kwa pointi 46 itawakaribisha Mbao FC kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi. Timu zote hizo hazina inachogombea zaidi ya kutafuta ushindi wa heshima.
Lakini zaidi Mbao FC yenye pointi 30 inahitaji ushindi kujiondoa katika hatari ya kushuka daraja. Kwani nafasi iliyopo ya 12 ni hatari kwake kutokana na kufanana na timu nyingine na kwa tofauti ndogo ya pointi hivyo, akifungwa na wengine wakishinda atakuwa hatarini zaidi.
Ruvu Shooting yenye pointi 32 itacheza na Kagera Sugar yenye pointi 46 zaidi anayetakiwa kupambana na kushinda ni Ruvu. Hata Kagera kama inataka kuendelea kumaliza ligi katika nafasi tatu za juu anahitaji kushinda.
Michezo mingine itakayochezwa leo ni Toto African yenye pointi 26 dhidi ya JKT ruvu yenye pointi 23. Huu pia huenda ukawa ni mchezo mgumu kwa kila mmoja kutokana na kwamba wote wanashikilia mkia wakiwa hatarini kushuka daraja. Majimaji yenye pointi 26 inatarajia kucheza na Mwadui yenye pointi 35.
Mchezo huo ni muhimu kwa Majimaji kushinda na kujiondoa kwenye hatari ya kushuka daraja.

Jumatano, 8 Machi 2017

Rais Magufuli na mkewe wawasili mkoani Dodoma

Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, amewasili Mkoani Dodoma ambako pamoja na mambo mengine ataongoza Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Mkutano Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi.

Mhe. Dkt. Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM ataongoza kikao na mikutano hiyo kuanzia tarehe 10 - 12 Machi, 2017 Mjini Dodoma.

Mhe. Rais Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli waliwasili jana katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma akitokea Mkoani Morogoro ambako jana tarehe 06 Machi, 2017 alizindua uwanja wa kisasa wa ndegevita wa Ngerengere.

SAA MBILI ZA MAANDAMANO WANAFUNZI BARIADI, Zilivyo simamisha mji wa Bariadi.

Wanafunzi wa shule ya sekondari Bariadi iliyoko katika halmashauri mjini wa Bariadi Mjini Bariadi wakiandamana katikati ya barabara kuu ya Bariadi-Lamadi, mjini Bariadi wakishinikizwa kurudishwa Mkuu wa shule yao ambaye alikuwa amepewa uhamisho Deus Toga, ambapo alikuwa amepelekwa shule ya sekondari Giriku na kuletewa Mkuu wa shule mwingine Paul Lutema ambaye walimkataa.


Mama Mlezi wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Afariki Dunia

 

Mama mlezi wa aliyekuwa Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Bi Nuru binti Halfani Shomvi amefariki dunia katika Hospitali ya Muhimbili alipokuwa akitibiwa asubuhi ya leo.

Kupitia mtandao wa twitter, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akishukuru jamii kwa salamu za pole alizopokea amesema shughuli za msiba ziko nyumbani kwa marehemu Mzee Kikwete, Mtaa wa Caravan, Bagamoyo na maziko yatakuwa Bagamoyo mjini, kesho Jumatano Machi 8, 2017 saa 10 Alasiri.

"Mama amefariki jana usiku saa nane, akiwa na miaka 91. Baba yangu, Mzee Halfani Mrisho Kikwete alikuwa na wake wawili alipofariki 1998. Mama yangu mzazi Bi Asha binti Jakaya, aliyekuwa mke mkubwa wa Mzee Halfani Kikwete alifariki 1999; tukabaki na mama yetu huyu mdogo". Kauli ya Jakaya Kikwete

Naye Mbunge wa Chalinze Mhe. Ridhiwan Kikwete ambaye ni mjukuu wa marehemu ndiye aliyekuwa wa kwanza kuthibitisha kutokea kwa kifo hicho asubuhi ya leo.

"Ndugu na marafiki nasikitika kuwatangazia msiba/kifo cha Bibi yetu Bi. Nuru Khalfan Kikwete kilichotokea asubuhi hii katika Hospitali ya Muhimbili alipokuwa amelazwa kwa matibabu. Taratibu za mazishi tutajulishana" Amesema Ridhiwan Kikwete.
 
Ndugu wapendwa, nawashukuru sana kwa salamu za pole na upendo kufuatia kifo cha Mama yangu mdogo mpendwa Bi Nuru binti Halfani Shomvi. – JK
— Jakaya Kikwete (@jmkikwete) March 7, 2017




CUF ya Maalim Seif kuiburuza CUF ya Prof.Lipumba mahakamani

Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF ), imefungua kesi ya madai dhidi ya wanachama wake nane akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya

Kesi hiyo imefunguliwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikitaka wanachama hao wasijihusishe na harakati  zozote za chama hicho.

Mbali ya Sakaya ambaye pia ni mbunge wa Kaliua mkoani Tabora, wadaiwa wengine ni Thomas Malima, mbunge wa Mtwara Mjini,Mafta Nachumu, Omar Mhina Masoud, Abdul Kambaya, Salama Masoud, Zainabu Mndolwa na Jafari Mneke.

Maombi hayo mbayo yametajwa mbele ya Hakimu Mkazi, Wilbard Mashauri yamewasilishwa na Wakili wa bodi, Hashim Mziray na yamepangwa kusikilizwa kesho.

Katika maombi hayo yaliyopewa namba 1 ya mwaka 2017, bodi inaiomba mahakama kutoa zuio kwa wadaiwa kutojihusisha katika masuala yeyote yanayohusiana na chama hicho.

Mbali ya maombi hayo, pia Wakili Mziray amewasilisha maombi madogo ya kuiomba mahakama kuwaamuru wadaiwa wasijihusishe na mikutano ya chama hicho.
 
Aidha, Mziray aliomba maombi yao madogo yasikilizwe kwa upande mmoja wa wadai tu kwa kuwa wamechelewa kuwapatia nyaraka za madai yao wadaiwa.

"Mheshimiwa tunaomba tusikilizwe upande mmoja ukizingatia maombi yameletwa chini ya hati ya dharula na kwa mujibu wa sheria mahakama hii... inayo mamlaka ya kufanya hivyo".

Hakimu Mashauri alisema anakubaliana na upande wa wadai na maombi hayo yatasikilizwa kesho mahakamani hapo.

Hatua ya Bodi ya CUF, kukimbilia mahakamani inakuja ikiwa ni siku moja baada ya upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hammad kupinga uteuzi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Uteuzi wa Profesa Lipumba ambao unapingwa ni ule alioufanya Machi 6, mwaka huu baada kuwaondoa katika nafasi zao, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Omar Ali Shehe.

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Salim Abdull Bimani, Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi, Abdullah Bakar Hassan.

Wengine ni Pavu Juma, Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadam na Sheria, Mahmoud Ali Mahindo na Katibu wa Jumuiya ya Vijana, Yusuph Salim.