ILULA YETU

ILULA YETU
HOME: ILULA YETU BLOG

Jumamosi, 6 Mei 2017

Yanga, Prisons kumekucha

View CommentsMABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Yanga leo wanashuka dimbani kuivaa Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi hiyo kusaka pointi tatu muhimu kuelekea kwenye harakati zao za kutetea taji hilo.
Mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga imetoka kupoteza mchezo wake wa nusu fainali Kombe la Shirikisho la Azam kwa kutolewa na Mbao FC baada ya kufungwa bao 1-0.
Huenda ikautumia mchezo huo kutafuta ushindi na kupoza machungu ya mashabiki wake baada ya kushindwa kusonga mbele hatua ya fainali ya michuano ya shirikisho. Katika mchezo wa raundi ya kwanza, Yanga ilishinda kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya bao 1-0.
Pia, katika mchezo wa robo fainali FA, Yanga iliwafunga tena Prisons mabao 3-0. Mchezo wa leo hautakuwa rahisi kwa pande zote Yanga ambaye anataka kupata pointi zitakazomsaidia kukimbizana na Simba kileleni kwenye msimamo, lakini pia, Tanzania Prisons ambao wana pointi 31 zisizotosha kuihakikishia kubaki salama.
Yanga yenye pointi 56 iwapo itashinda itafikisha 59 na kubakiza michezo minne mkononi, lakini kuna nafasi kubwa ya kupanda kileleni akiongoza kwa magoli mengi ya kufunga lakini iwapo Simba yenye pointi sawa na hizo 59 itashinda kesho dhidi ya African Lyon, basi Yanga itashuka nafasi ya pili.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema wachezaji wote wanaendelea vizuri na wapo tayari kwa mchezo huo. “Tunashukuru Mungu wachezaji wote waliokuwa Mwanza wanaendelea vizuri, tumejipanga kuhakikisha tunapata ushindi,”alisema.
Aidha, Azam FC inayoshika nafasi ya tatu kwa pointi 46 itawakaribisha Mbao FC kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi. Timu zote hizo hazina inachogombea zaidi ya kutafuta ushindi wa heshima.
Lakini zaidi Mbao FC yenye pointi 30 inahitaji ushindi kujiondoa katika hatari ya kushuka daraja. Kwani nafasi iliyopo ya 12 ni hatari kwake kutokana na kufanana na timu nyingine na kwa tofauti ndogo ya pointi hivyo, akifungwa na wengine wakishinda atakuwa hatarini zaidi.
Ruvu Shooting yenye pointi 32 itacheza na Kagera Sugar yenye pointi 46 zaidi anayetakiwa kupambana na kushinda ni Ruvu. Hata Kagera kama inataka kuendelea kumaliza ligi katika nafasi tatu za juu anahitaji kushinda.
Michezo mingine itakayochezwa leo ni Toto African yenye pointi 26 dhidi ya JKT ruvu yenye pointi 23. Huu pia huenda ukawa ni mchezo mgumu kwa kila mmoja kutokana na kwamba wote wanashikilia mkia wakiwa hatarini kushuka daraja. Majimaji yenye pointi 26 inatarajia kucheza na Mwadui yenye pointi 35.
Mchezo huo ni muhimu kwa Majimaji kushinda na kujiondoa kwenye hatari ya kushuka daraja.